Wednesday 12 June 2013

SHIWATA yandaa Tamasha la Kimataifa Dar.


MTANDAO wa Wasanii Tanzania (SHIWATA) umeandaa Tamasha la Kimataifa la Michezo mbalimbali litakalofanyika Juni mwaka huu kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Tamasha hilo limeandaliwa ili kupata fedha za kujenga nyumba za wasanii katika kijiji cha Mwanzega, Mkuranga.


Mwenyekiti wa SHUWATA, Caasim Taalib alisema jana kuwa kutakuwa na michezo na burudani mbalimbali kutoka Tanzania, India, Marekani, Uingereza, Ujerumani, China watakaonesha ustadi wa kucheza katika utamaduni wa nchi zao.


Taalib alisema pia kutakuwa na michezo mipya iliyobuniwa na mtandao huo kama SHIWATA Basketball, SHIWATA Football ambayo inachezwa na ngongoti pia kutakuwa na ngoma, kwaya,Bongo Fleva, dansi, mieleka na michezo mingine ambayo itatoa burudani ya kutosha.


Alisema pamoja na wanachama 185 wa SHIWATA kuamua kuchangisha sh. 200,000 kila baada ya miezi mitatu kwa ajili ya ujenzi wa nyumba hizo,mtandao huo umeamua kutafuta fedha zaidi kwa njia ya matamasha na filamu ili kuwapunguzia mzigo wa kujichangisha.


Mwenyekiti Taalib alisema mapato ya tamasha hilo yatawanufaisha wanachama 185 ambao tayari wameonesha nia ya kujenga nyumba hizo kupitia filamu iitwayo Kisufuria iliyokwisha chezwa na sasa inahaririwa.


Alisema matamasha kama hilo yanatarajiwa kufanyika katika mikoa ya Mwanza, Arusha, Dodoma, Morogoro,Ruvuma, Tanga na Zanzibar ili kujenga nyumba 1,000 kama inavyokusudiwa.


"Nyumba tano zilizojengwa katika awamu ya kwanza na nyumba 180 zinazotarajiwa kuanza kujengwa awamu ya pili Julai mwaka huu, tunawahimiza wanachama wote kuchangia ujenzi wa nyumba zao ili waweze kufaidika kwa fedha zitakazokusanywa kutokana na filamu ma matamasha yaliyoandaliwa"alisema Mwenyekiti Taalib.




No comments:

Post a Comment